Hakuna Pazia. Ukweli Haufichiki.
Kwa nini?
Kila safari huanza na swali moja tu: Kwa nini? Wengi wanajishughulisha na "Nini" au "Vipi," lakini wanaolenga mafanikio wanajua kwamba “Kwa nini” ndio msingi wa yote. Kwa hivyo, mimi pia ninaanza hapo.
"Mtume Muhammad (saw) alisema: “Dini ni naseeha (ushauri, ikhlasi).” Tukauliza: “Kwa nani?” Akajibu: “Kwa Mwenyezi Mungu, Kitabu Chake, Mtume Wake, na kwa viongozi wa Waislamu na watu wao wote.” [Imepokewa na Muslim]
Kwa nini ninaandika? Kwa sababu ninaamini kwamba ikhlasi - ushauri wa kweli, ndiyo msingi wa dini, na ndiyo msingi wa jamii yenye haki.
Kwa nini nimechagua jina “Hakuna Pazia?" Kwa sababu ninaamini kwamba uwazi, ujasiri, na ukweli ndivyo vinavyoweza kuwaokoa watu.
Kwa nini siandiki kwa ajili ya umaarufu wala ya pesa? Ninaandika kwa sababu ninaamini - ninaamini kwamba kuna pazia kubwa inayofunika macho ya watu – pazia ya ufisadi, ukimya na hofu. Na wajibu wangu ni kuipasua.
Kwa nini nipo hapa mtandaoni? Kuonyesha ukweli kwa kuipasua pazia ili kutimiza naseeha.
Vipi?
Siandiki kwa hisia tu - naandika kwa uchunguzi, ushahidi, na moyo wa ikhlasi. Kila makala ninayoandika inapitia hatua zifuatazo:
1. Uchunguzi - Kutafiti taarifa za vyanzo nilivyoweza kuvipata.
2. Uchanganuzi Wazi na Huru - Kuchanganua kwa kina kusikoegemea mrengo fulani.
Naseeha - Kila makala ni ushauri wa kweli kwa viongozi na wananchi jumla - si kwa ajili ya kuburudisha, bali kwa ajili ya kuzisukuma au kuziamsha akili ziweze kuleta mabadiliko.
Nini?
Ninaandika masuala muhimu yanayoikabili jamii yetu na dunia kwa ujumla. Baadhi ya mada ninazozishughulikia zinajumuisha sio tu: Siasa, Uchumi, Elimu, Usalama wa Kidijitali na Mitandao nk.
Kila makala inalenga: kuhamasisha mawazo, kuhamasisha hatua na kuleta mabadiliko.
Sauti Yangu
Hakuna Pazia si mradi wa mtu mmoja - ni harakati ya pamoja.
Mafanikio makubwa hayatokei kwa bahati; yanatokana na watu wanaojua "Kwa nini" wanaamka kila asubuhi. Wewe ni sehemu ya ile naseeha kwa jamii - ushauri wa kweli unaohitajika.
Katika ulimwengu wa leo, pazia kuu ni: Taarifa potofu, Ukimya wa kimakusudi na Hofu ya kusema ukweli.
Mimi nimechagua kuipasua pazia hiyo kwa sababu ninaamini kwamba ukweli, hata uwe uchungu kiasi gani, ndio tiba ya taifa. Mwenyezi Mungu (SWT) asema:
“Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” [Al-Maidah 5: 119]
Mtume Muhammad SAW alisema kupitia Abu Dhar (RA):
"Sema ukweli hata kama ni uchungu.” [Imepokewa na Ibn Hibban]
Kila unaposoma, unapojadili. unaposambaza makala zangu, unakuwa sehemu ya harakati hii.
Naomba ujiulize: Kwa nini unasoma? Kwa nini unajali? Kwa nini unataka kuona pazia ikipasuka?
Tumia jibu lako kuwa sehemu ya mabadiliko.
Karibu
Usinyamaze kimya, uliza maswali na kumbuka: Hakuna Pazia. Ukweli Haufichiki.
Kwa pamoja, kwa ujasiri na ikhlasi, tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli yenye ustawi wa kweli.
The team









